Kupitia mtandao wa kijamii wa Truth Social, Trump ameandika: “Nchi yoyote itakayofuata sera za BRICS zinazopinga Marekani, itatozwa ushuru wa ziada wa asilimia 10. Hakutakuwa na msamaha wowote katika sera hii.”
Kundi la BRICS, liianzishwa mwaka 2009 na Brazil, India, Russia na China, huku Afrika Kusini ikijunga mwaka mmoja baadaye. Mwaka huu kundi hilo limepanuka na kujumuisha Saudi Arabia, Misri, Ethiopia, Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu, na Indonesia.
Tishio la Trump limetolewa wakati ambapo BRICS—inayojumuisha zaidi ya asilimia 40 ya watu duniani na karibu asilimia 30 ya pato la taifa la dunia (GDP)—imekuwa jukwaa muhimu kwa mataifa yanayotafuta mfumo wa haki zaidi wa kiuchumi. Nchi nyingi zinazojiunga na BRICS hutafuta njia mbadala ya mfumo unaotawaliwa na sarafu ya dola ya Marekani, kwa lengo la kujenga ukuaji wa kiuchumi unaojitegemea.
China na India zikiwa nguvu kuu za Asia, pamoja na mataifa yenye utajiri wa nishati kama Russia, Saudi Arabia na Iran, zimeunda muungano wa kiuchumi na kijiografia wenye uwezo mkubwa wa kujitegemea bila kutegemea masoko ya Magharibi.
Katika hali hii, tishio la Trump linaweza kuonekana kama jaribio la kudumisha nafasi ya Marekani katika mfumo wa dunia, lakini kwa hakika linaweza kuleta athari za kinyume:
Kwanza, linakiuka misingi ya biashara huria ambayo Marekani imekuwa ikitetea kwa miongo kadhaa.
Pili, linaweza kuhimiza mataifa zaidi kuachana na utegemezi wa mfumo wa kifedha wa Magharibi na kujiunga na miungano mbadala kama BRICS.
Kwa upande mwingine, mataifa mengi yanayoshirikiana na BRICS kwa sasa yanageuka kuwa vituo vipya vya ukuaji wa kiuchumi. Kwa mfano, nchi za Ghuba ya Uajemi ambazo zimejiunga hivi karibuni na BRICS zina rasilimali nyingi za nishati na uwezo mkubwa wa uwekezaji—na ni washirika muhimu wa nchi za Magharibi. Kuwatishia kwa ushuru kunaweza kuwasukuma zaidi kuelekea mashariki na hivyo kupunguza utegemezi wao kwa soko la Marekani.
Faida za kushirikiana na BRICS ni nyingi: Kupata washirika wa kibiashara mbadala. Upatikanaji wa fedha kutoka taasisi zisizo za Magharibi. Ushirikiano katika sekta za nishati, teknolojia na miundombinu
Ulimwengu wa leo si sawa na ule wa miaka ya 1990 au mwanzoni mwa miaka ya 2000 ambapo Marekani ingeweza kuamua mwelekeo wa uchumi wa dunia kwa vitisho na ushuru. Mataifa yanayoibukia sasa yanaunda mifumo mipya ya kifedha na kibiashara inayopunguza utegemezi kwa dola ya Marekani. China na Russia tayari zimeanza kutumia sarafu za kitaifa katika biashara ya kimataifa—na mwelekeo huu hautasimama kwa sababu ya vitisho vya ushuru.
Kwa ujumla, tishio la Trump si tu kwamba halina msingi wa kiuchumi, bali linaashiria jitihada za mwisho za kulinda mfumo wa dunia usio na usawa. Katika dunia inayozidi kuwa ya mwelekeo wa pande nyingi, kila taifa lina haki ya kuchagua washirika wake wa kiuchumi kwa kuzingatia maslahi ya kitaifa, na sio mashinikizo ya dola moja. BRICS sasa inajitokeza kama kundi ambalo ni mhimili mkuu wa mfumo mpya wa kiuchumi wa dunia, na hakuna ushuru wowote utakaoweza kuzuia mabadiliko haya.
Your Comment